Watumishi wa Umma ndani ya mkoa wa geita wamekumbushwa juu ya misingi mbalimbali ya utumishi ndani ya serikali huku wakionywa kuhusu kuepuka kuichonganisha serikali na wananchi wake kupitia huduma wanazozitoa.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Utawala wa Utumishi wa Umma kutoka Ofisi ya Rais-Ikulu Bw. Francis Mang’ira Julai 29, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wakati akiwasilisha maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa watumishi wa sekretarieti ya mkoa, hospitali ya mkoa na wakuu wa taasisi za umma mkoani hapa.
“kila mtumishi wa umma kwa nafasi yako hakikisha hauichonganishi serikali na wananchi kwa kuhakikisha kila mwananchi anapofika kupata huduma katika ofisi za umma anapokelewa, anasikilizwa na kuhakikisha anaelekezwa sehemu husika hata kama shida yake si ya ofisi uliyopo”. Amesema Bw.Mang’ira.
Ameendelea kueleza kuwa, watumishi wa umma hawatakiwi kuchanganya masuala ya siasa wanapotekeleza majukumu yao ili kuepuka upendeleo, uonevu, usumbufu n.k huku akisisitiza juu ya kumhudumia mwananchi katika ubora, usahihi, haki, bila upendeleo na ubaguzi.
Pamoja na hayo, watumishi pia wame elekezwa kuhakikisha wanafanya kazi na kuepuka majungu na kutoingilia majukumu ya wenzao wakihimizwa kila mmoja kuhakikisha anakuwa na malengo na mikakati ya utekelezaji wa kazi zake katika kuhakikisha huduma stahiki zinamfikia mwananchi huku akikemea tabia ya viongozi wa ngazi za chini wanaouza huduma kwa wananchi ambazo tayari serikali imekwisha kuzilipia.
Kwa upande wake Bw.Abdallah Mnongane ambaye ni Mratibu Msaidizi wa Utawala wa Utumishi wa Umma Kutoka Ofisi ya Rais-Ikulu amesisitiza juu ya uzingatiaji wa SHERIA, TARATIBU na KANUNI (STK), bila kusahau miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi.
Bw. Mnongane amehimiza juu ya idara, vitengo na taasisi kuwa na utamaduni wa kufanya vikao hata mara mbili kwa mwezi ili viwezeshe kutoa mrejesho wa utendaji, vilevile kuwa kama chombo cha kuibua changamoto na kero za watumishi na si kupeleka kero zao nje ya ofisi.
Kuheshimu madaraka, kuzingatia maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma, nidhamu, kushughulikia malalamiko ni sehemu ya yaliyoelekezwa na Bw. Mnongane akisema watumishi ni vyema kuyazingatia.
Maelekezo hayo yanaendelea kutolewa kwa watumishi wa umma ndani ya mkoa wa geita ambapo hadi sasa tayari yamefikishwa kwa watumishi walioko wilaya ya Geita, Chato, Nyang’hwale na Bukombe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa