Idara ya Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita imeendesha mafunzo ya awali kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 07-08.07.2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ili kuwajengea uwezo watumishi wa umma kwa zaidi ya ishirini kutoka ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA). Mafunzo haya ni kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 toleo la tatu Kanuni G.1 (8) inayomtaka kila mwajiri kutoa Mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) Mhandisi Frank Changawa aliwaambia washiriki wazingatie mafunzo watakayopewa kwani ni kwa manufaa yao kwa kuwa wengi wao ni vijana na ni wageni katika utumishi wa umma.
Mafunzo hayo yaliyohusisha waajiriwa wapya Wasoma Mita za Maji, Wahandisi wa Maji, Mafundi Bomba, Wahasibu, WaTEHAMA, Maafisa Usafirishaji, na Maafisa Utumishi yaliwezeshwa kupitia mada mbalimbali zikiwa na msingi uliowataka kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni (STK) kama watumishi wa umma.
Mada zilizotolewa ni pamoja na Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma iliyowezeshwa na Bw. Mteule Mnyalape - Afisa Utumishi, ambaye aliwaeleza washiriki kuwa; kama Mtumishi wa Umma ni lazima kutimiza wajibu ili kupata haki. Bw. Mnyalape aliwapitisha washiriki kwenye Kanuni za Maadili ya Utendaji Katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005 zilizohusisha tabia na mienendo ya kimaadili, kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, Bidii ya kazi, matumizi sahihi ya taarifa kutoa huduma bila upendeleo n.k
Bw Masoud Biteyamanga ambaye ni Afisa Tawala Mkuu aliwasilisha mada inayohusu Uendeshaji wa Ofisi ambapo aliwaeleza washiriki kuwa, kama watumishi wa umma wanatakiwa kuufahamu mfumo wa mawasiliano serikalini, mahusiano kazini au taasisi nyingine, kutunza siri, utunzaji wa majalada, tabia za mtumishi wa umma, namna ya kupokea maagizo kwa barua, pamoja na namna ya kupokea simu. Aliongelea Itifaki kwa watumishi hao na kuwaasa kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza endapo utaratibu uliowekwa na taasisi yao hautafuatwa.
Kwa upande wake Afisa Tawala Bi. Beatrice Masanja alihimiza suala la utunzaji rasilimali za umma na kuwaonya watumishi hao kutumia vibaya nyaraka za serikali. Hii ni pamoja na kuona vitendea kazi kama gari, kompyuta, swichi za umeme n.k vinatunzwa ili kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza mfano pale Afisa Usafirishaji.
Akiwaelekeza namna ya ujazaji wa Fomu ya Upimaji wa Wazi (OPRAS), Bw. Herman P. Matemu, Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimali Watu ambaye pia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita aliwaeleza watumishi hao kuwa ni lazima kujaza fomu hizo kwani ndio mkataba wa utendaji kazi kwa mwaka ili iwawezeshe msimamizi wao wa kazi (Mkuu wa Taasisi/Mamlaka) kutathmini utendaji kazi wao kwa kipindi husika na kuwa taarifa zinazojazwa kwenye fomu hiyo humfanya mtumishi kuwajibika.
Akiongea kwa niaba ya waliopokea mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa GEUWASA Mhandisi Isaack Joseph Mgeni aliwashukuru kwa ushirikiano uliooneshwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa kuwa sehemu ya kufanikisha mafunzo hayo kupitia wakufunzi yaliyowajenga watumishi anaowasimamia jambo lililopelekea Afisa Utumishi wa Mamlaka hiyo Bi. Audrian Chitama kuahidi kuyafanyia kazi kwa kusimamia utekelezaji wa yote waliyoelekezwa na wakufunzi kisha Kaimu.
Kisha Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Herman P. Matemu aliwapongeza washiriki kwa namna walivyoshiriki kikamilifu kupitia mahudhurio, umakini na nidhamu walioionesha wakati wa mafunzo lakini pia kuwapongeza menejimenti ya GEUWASA kwa kutenga muda ili kuwapa watumishi wake mafunzo hayo muhimu ili yatumike kama ilivyotarajiwa na kufunga mafunzo hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa