Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 Ndugu. Ismail Ali Ussi ametoa hamasa kwa wawekezaji wa ndani kutumia vyema fursa zilizowekwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwekeza katika miradi ya sekta mbalimbali za kijamii ikiwemo shule, hospitali na nyinginezo.
Ndg. Ismail Ali Ussi ametoa kauli hiyo tarehe 4 Septemba 2025 alipokuwa akizungumza na hadhira iliyojitokeza kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Gakala kilichopo Wilayani Mbogwe na kinamilikiwa na mwekezaji mzalendo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 ameeleza namna alivyofarijika kuona dhana ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya watanzania wenyewe kuijenga Nchi yao inatekelezwa na wawekezaji wachache wanaojitoa kuwekeza katika miradi inayotoa huduma za kijamii na kuongeza ajira za wananchi wa maeneo husika ambao wameajiriwa katika miradi inayoanzishwa na wawekezaji.
“Mwenge wa Uhuru umewaheshimisha wananchi wa Mbogwe kupitia mradi huu mkubwa na sasa huduma za afya katika Wilaya ya Mbogwe zimezidi kuboreshwa baada ya mwekezaji mzalendo mwenye tija ya kuijenga Nchi yake ameamua kuonyesha kwa vitendo kwa kuwekeza kwenye sekta ya afya badala ya miradi mingine yenye mlengo wa kujiingizia kipato binafsi kikubwa.” Aliongeza Ndg. Ismail Ali Ussi.
Ndg. Ismail Ali Ussi ameongeza kuwa mwekezaji huyo ameondoa hofu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla katika upatikanaji wa huduma zote katika Kituo cha Afya Gakala ikiwemo huduma ya kujifungua ambayo ni muhimu sana katika utatuzi wa changamoto ya vifo visivyotarajiwa vya kina mama na watoto wachanga kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo muhimu kwa haraka na karibu na makazi yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Afya Gakala Ndg. Bunga Dadu amesema kuwa lengo la ujenzi huo ni kusaidia wananchi wa Kata ya Bukandwe na kata jirani kupata huduma bora za afya za kibingwa jirani na makazi yao.
Ndg. Bunga Dadu ameeleza kuwa ujenzi wa Kituo hicho wenye thamani ya shilingi Bilioni tatu ulianza rasmi mwezi Disemba mwaka 2024 kwa hatua ya kwanza ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje( OPD), jengo la mama, baba na mtoto, jengo la utawala, nyumba ya watumishi, jengo la upasuaji, kichomea taka na shimo la kutupia kondo la nyuma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa