Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) na Mgeni Rasmi wa Jukwaa la Fursa za Biashara Mkoani Geita amezidi kuinua ari ya wanageita pale alipoutangazia Mkoa neema kwenye maeneo makuu matatu alipokua akihutubia washiriki wa Jukwaa la Fursa za Biashara kwenye ukumbi wa GEDECO uliyopo Halmashauri ya Mji wa Geita tarehe 16.08.2018 jambo lilipongezwa sana na Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mhe. Dkt. Mwakyembe ameushauri Mkoa kuhakikisha unatenga asilimia moja 1% ya fedha za Miradi ya Huduma kwa Jamii (CSR) zinazopatikana kila mwaka kwa ajili ya kuendeleza michezo.
Baada ya kutambulishwa kwa Miss Geita 2018 Bi. Joyce Magesa mbele ya mgeni rasmi na kupewa nafasi kuongea na washiriki wa jukwaa hilo, Mhe.Waziri alisema “ifike mahali shirika letu la ndege tuwatumie walimbwende wetu kuwa watumishi ndani ya ndege;, “hii ni namna nzuri ya kukuza fani hii. Awali wengi walifikiri urembo ni uhuni lakini kupitia mkoa wa Geita, Miss Geita sasa amekuwa mfano kuonesha kuwa hata urembo ni ajira na ni fani kama zilivyo nyingine pale alipofika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita kuomba apangiwe majukumu kuihudumia jamii ya Geita, hili ni jambo jema”, aliongeza.
Dkt. Mwakyembe pia akaiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwatumia walimbwende kudai madeni, jambo litakalowaongezea ufanisi katika makusanyo, lakini vile vile kuhakikisha utaratibu wa utoaji stika kwa kazi za wasanii unafika mikoani kuondoa usumbufu.
Mhe. Waziri alitembelea uwekezaji wa kiwanda cha kuchakata na kuchenjua madini ya dhahabu cha Jema Africa Elution kilichopo eneo la Nyanza Mtaa Mbugani na kuona shuguli zinazofanyika kisha kuutembelea uwanja wa michezo unaotarajiwa kujengwa wa Magogo Mjini Geita kisha kuahidi kuwatuma wataalam kuja Geita kupima na kutoa ushauri ili uwanja uwe bora na wa kisasa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru sana Mhe. Waziri kwa kukubali kuwa mgeni rasmi pia kushiriki mwanzo hadi mwisho wa Jukwaa la fursa za biashara, lakini pia TSN kwa ushiriki wao katika kufanikisha jukwaa hilo bila kuwasahau wadhamini wote akiwemo mdhamini mkuu GGM.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Dkt. Hassan Abbas ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya TSN akatumia fursa hiyo kuuhakikishia umma wa Geita na Tanzania kuwa ndani ya muda mfupi kuanzia sasa, Serikali itatangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa daraja kwenye kivuko cha Kigongo Busisi ili kurahisisha usafiri kwa watumiaji wa kivuko hicho, “Tunatekeleza” alimalizia.
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali TSN Bi. Tuma Abdallah kipekee akaushukuru uongozi wa Mkoa kupitia Mkuu wa Mkoa akisema kuwa “tangu TSN imeanza juhudi zakufanya majukwaa ya fursa za biashara, Jukwaa la Geita limekua la mfano na la kihistoria na limeafanyika zaidi ya siku moja tofauti na mikoa mingine”. Hivyo akaendelea kushauri wadau wa maendeleo kuzitumia fursa zilizopo ili kufanya mabadiliko ya kimaendeleo.
Jukwaa hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa Alhaj Said Kalidushi, Katibu Tawala wa Mkoa ndugu Denis I. Bandisa, Naibu katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni mwasisi wa jukwaa la fursa za biashara, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndugu Richard Kayombo, Wahe.Wakuu wa Wilaya za Geita, Wahe Wabunge, Wahe. Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Makatibu Tawala, Madiwani, Wakuu wa Idara pamoja na Maafisa Habari Mkoa wa Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa