Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Said Jaffo (Mb) amepongeza juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Geita kupitia Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel za usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo alipotembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Soko, Barabara na Vituo vya Kutolea Huduma za Afya tarehe 09.08.2018 ili kuona utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa mara ya mwisho alipotembelea miradi hiyo tarehe 13.05.2018.
Ametembelea Mradi wa Ujenzi wa soko Halmashauri ya Mji Geita lenye miundombinu ya Mama na Baba Lishe na kisha kupata maelezo ya Mkurugenzi wa Mji Geita Eng. Modest Apolinary na kusema, “niwapongeze kazi nzuri, na kwakuwa nimekutana na wakuu wa idara karibu wote, niwapongeze hasa kwa ukusanyaji wa mapato, kwani hili limenipa faraja sana, inaonekana Geita imejipambanua na mko makini kwenye ukusanyaji wa mapato na kwa staili hii, mnatakiwa kuwa katika levo ama hatua nyingine ya juu zaidi. Lakini pia naomba muendeleze mahusiano mazuri kwani hayo ndiyo yamepelekea mafanikio mzuri kwakuwa mnao viongozi wachapa kazi kuanzia Mkuu wa Mkoa mpaka Wakurugenzi hivyo nataka Geita iwe sehemu ya watu kuja kujifunza na nimeridhika na mradi huu”, alimaliza.
Ametembelea pia ujenzi wa barabara ya American Chips-Katundu ya kiwango cha Lami na yenye urefu wa Km. 2.4 na kupongeza ujenzi wa daraja na kutoa agizo la kuzingatia usafi na utunzaji wa mazingira kwenye miundombinu hiyo ili baadae isizibe na ikiwezekana kuweka adhabu kwa watakaotupa taka kwenye mitaro au madaraja, kisha kuendelea na ziara yake wilayani Chato.
Akiwa Chato ametembelea Zahanati ya Buselesele iliyoko Kata ya Buselesele na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato kuhakikisha jengo la kujifungulia akina mama linakamilika ili kupunguza msongamano. Ameongea na wananchi na kutangaza neema kwao akisema “nimekuja kuwatembelea Mkoa wa Geita, kwenye zahanati yenu nimeona hali yenu si nzuri, na kwakuwa Mhe. Rais amenipa dhamana, nipo barabarani kuangalia matatizo ya wananchi na hapa mpo wengi nami nasema tutahangaika kwa kadri iwezekanavyo, serikali itatafuta fedha, tuje kujenga kituo cha kisasa zaidi katika Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Buselesele kwa sababu haiwezekani Mhe. Rais ahangaike, halali alafu wananchi wake wapate tabu hivyo basi nikuombe Mkuu wa Mkoa fedha hizo zikifika zisimamiwe ndani ya muda mfupi Kituo hiki cha Afya kiwe kimekamilika ili wananchi watibiwe vizuri na kumaliza.
Pia amewaomba wananchi hao waendelee kumuombea Mhe. Rais Afya njema ili aendelee kuwatumikia, kisha msafara wake ukaelekea kituo cha Afya Bwanga ambapo ameridhika pia na ujenzi wa miundombinu ya afya katika kituo hicho na kuwataka watumishi kuwa wabunifu katika kutafuta namna ya kupunguza msongamano kwa wananchi wanaopata huduma kwenye kituo hicho na baadaye msafara wake ukaelekea Shule ya Sekondari Magufuli.
Akiwa Shuleni hapo, Mhe.Waziri Jaffo ameongea na kusalimiana na wanafunzi pamoja na walimu kisha kuwapongeza kwa kuwa nafasi ya kumi na nane kitaifa (18) na kutoliaibisha jina kubwa ambalo shule hiyo imelibeba. Alisema “kitu kilichonifanya nije ni hapa ni kwa sababu shule yenu imefanya vizuri katika Shule za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika matokeo ya kidato cha sita kitaifa. Shule yenu ni ya mfano sasa ukizingatia ni ya kawaida hivyo ni jambo la kujivunia mnastahili pongezi. Walimu wenu kumi na nane (18)wamefanya kazi kubwa sana nao wanastahili pongezi”.
Akaongeza kwa kusema, “Mkuu wa Mkoa, angalia uwezekano, hawa waalimu wafanyiwe sherehe maalumu ya kimkoa kama walimu wa heshma walioleta heshma ndani ya mkoa”, na akawaeleza wanafunzi wa kidato cha kuhakikisha kuwa kuanzia siku anatoka shuleni hapo mpaka wanaingia kwenye mtihani waimbe wimbo wa kizalendo maana nataka mwakani wawe kwenye shule kumi bora za Tanzania. Awatahadharisha watakapo muona mwenzao anateleza basi wamrekebishe ili wafaulu kwa pamoja na kuahidi kuwafanyia sherehe endapo mwakani watapata wote daraja la kwanza, aomba shule hiyo isaidiwe kwa namna yoyote ili iendelee kufanya vizuri kwani ni tunu ya mkoa.
Kisha Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel akashukuru kwa ugeni wa Mhe. Waziri na kuhaidi kutekeleza yake yote yaliyoagizwa ili kuleta tija kwa wananchi wa Geita na Tanzania kwa ujumla kisha Mhe.Waziri kuendelea na ziara yake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa