Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ameendelea kugusa mioyo ya Watanzani kwa kukemea tabia ya baadhi ya watumishi ambao bado ni wazembe na kujifanya miungu watu katika kusimamia fedha za umma na miradi ya maendeleo nchini akiwa katika mkutano wa hadhara kwenye eneo la Shule ya Sekondari ya Buselesele, Kata ya Buselesele, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi tarehe 20.10.2018.
Waziri Jafo ameanza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kwa jinsi anavyolitumikia Taifa kwa kuwajali Watanzania wenye hali duni akiwawekea miundombinu mbalimbali ikiwemo ya afya na elimu.
Ilimlazimu Waziri Jafo kusema,“Mhe. Rais kupitia TAMISEMI amefanya mapinduzi makubwa ya kihistoria, kwakuwa tangu Nchi yetu inapata Uhuru hadi mwaka 2010, tulikuwa na Vituo vya Afya Mia Moja Kumi na Tano (115) pekee vyenye uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji, hivyo aliniagiza kufanya kazi kubwa katika eneo hilo ambapo leo hii ndani ya Miezi Kumi na Nane (18) tunakamilisha vituo vya afya Mia Tatu Arobaini na Tano (345) kwa mara ya kwanza katika nchi hii. Hivyo huyu ni Rais ambaye viatu vyake inawezekana ikapita miaka mingi sana kuvaliwa na mtu mwingine”. Asante Mhe. Rais.
Pamoja na shukrani hizo, Waziri Jafo amewafuta machozi ya wakazi wa Buselesele kwa kuwahakikishia ujenzi wa Kituo cha Afya Buselesele kabla ya mwezi Desemba 2018 na kwamba, hayos ndiyo matunda ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema kuwa, tayari Wizara imeleta Shilingi Milioni Mia Saba (Tshs.700, 000,000/=) kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mbuye, Kijiji cha Mbuye Kata ya Bwina Wilayani Chato. Vile vile Shule ya Sekondari ya Buselesele itapewa Shilingi Milioni Mia Mbili Hamsini (250,000,000) ndani ya mwezi Oktoba, 2018 ili Shilingi Milioni Mia Moja (100,000,000) zijenge Bwalo kubwa, na yajengwe Mabweni (Hostel) mawili yenye kugharimu Shilingi Milioni Sabini na Tano (75,000,000/=) kila moja yakiwa na vitanda vyake na fedha zitakapoingia ujenzi uanze mara moja ili mwezi Juni mwaka 2019 kianze kidato cha tano kama lilivyokuwa ombi la wananchi wa Buselesele. Kisha Mhe. Jafo akamuagiza Mkurugenzi wa Chato kuhakikisha anasimamia Halmshauri vizuri ili fedha zinapoingia kazi ianze na kukemea utendaji kazi wa kizembe na kutoa hadi mwezi wa pili, 2019 mabweni na bwalo viwe vimekamilika.
Kwa motisha zaidi, Shule ya Sekondari Magufuli iliyopo Kata ya Bwanga Wilayani Chato imepongezwa na kuahidiwa kupewa Milioni Hamsini (Tshs. 50,000,000/=) kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba nzuri ya kujisomea kufuatia matokeo mazuri ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2018 kama shule ya serikali kwa kuwa shule ya 18 kati ya shule bora kitaifa 20. Mwisho Waziri Jafo amewasisitiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano huku akipongeza juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel kwa usimamizi mzuri.
Naye Mhe. Dkt. Medard Kalemani, Mbunge wa Chato na Waziri wa Nishati akamshukuru Mhe. Jafo kwa kukubali kufanya ziara Wilayani Chato na kisha akatoa baiskeli ya miguu mitatu kwa mwananchi mwenye ulemavu aitwaye Mama Makumila kama chombo kitakachomsaidia usafiri.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe.Mhandisi Robert Gabriel alimkaribisha Waziri Jafo, akimpongeza na kumshukuru Mhe. Rais kisha Kumhakikishia kuwa ataendelea kuisimamia Geita ili ifanane na Dhahabu iliyopo na kwamba wezi hawana nafasi Gieta.
Mhandisi Gabriel amesema kwamba, tayari ameandaa ziara Kijiji kwa Kijiji, Kata kwa Kata akiapa kuusafisha Mkoa kwa kuwaondoa walaji wote na kwamba itakua ziara ya kwanza maalumu kwa ajili ya kuusafisha mkoa kwa lengo la kuthibiti fedha za umma, kisha Mhe. Jafo akaendelea na ziara yake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa