Imeelezwa kuwa, jumla ya Tshs.167, 972,000 zitazinufaisha kaya 2,919 zinazoendelea kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ndani ya Halmashauri ya Mji Geita ikiwa ni kipindi cha tatu cha uhawilishaji fedha tangu kuanza kwa mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya pili TASAF III- PSSN II.
Hayo yamebainishwa Aprili 14, 2021 na Mratibu wa TASAF Mkoa wa Geita Bw. Elikana Haruni alipokuwa katika ziara ya kufanya mikutano ya uamsho katika mitaa ya Geita Mji iliyopo kwenye kwenye mpango huo wakati wa uhawilishaji wa fedha huku akihimiza ufikiwaji wa malengo ya mpango, kuwahimiza wanufaika hao juu ya utekelezaji wa masharti ya mpango, kujisajili ili kupokea fedha kwa njia ya simu, lakini vilevile kusikiliza kero na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo walengwa.
Bw. Haruni amewaeleza wanufaika hao kuwa, inawapasa kuzingatia masharti ya elimu na afya kila wapatapo fedha hizo ili kuhakikisha zinawasaidia watoto wanaowalea na kuwatimizia mahitaji yao kupitia fedha hizo kisha kutumia kiasi bakia kujiimarisha kiuchumi ili kuondokana na sifa ya umasikini uliokithiri. Vilevile, wanufaika hao wamesisitizwa juu ya kusajili namba zao za simu ili waweze kupokea fedha hizo kwa njia ya simu ya mkononi ili kuondoa usumbufu wakati wa kupokea huku wakionywa kutumia simu zao kukopea fedha mitandaoni na baadaye kuona kama fedha hizo hazijawekwa baada ya kukatwa kwenye mitandao ya simu.
“nimeona niwakumbushe juu ya masharti ya mpango, kuwahamasisha ambao hamjasajili namba zenu kwaajili ya kupokea fedha kwenye simu lakini pia muepuke kutoa namba zenu za siri mkiwapa vijana wenu ambao wengine hutumia namba zenu kukopea fedha, na endapo zikatumwa basi zitakatwa na mitandao husika nanyi mtapata fedha pungufu, hivyo muwe makini” alisema bw Haruni.
Akihitimisha, mratibu Haruni ameonya wapokeaji wa fedha wenye tabia ya kuwatenga wenza wao akisisitiza kuwa, TASAF huwaleta wenza karibu na isiwe chanzo cha familia kugombana kisa fedha wanazozipokea kupitia mpango.
Walengwa hao katika nyakati tofauti, wamemshukuru mratibu huyo kwa namna ambavyo amekuwa akiwatembelea na kutoa ufafanuzi juu ya mambo mbalimbali ambapo walengwa hao wameahidi kuendelea kuzitumia fedha hizo kama ilivyokusudiwa.
Itakumbukwa kuwa, mpango huu wa Kunusuru Kaya Masikini kipindi cha pili ulizinduliwa jijini Dodoma Februari, 2020 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli baada ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini awamu ya kwanza kukamilika.
Jumla ya mitaa 5 ya Mkolani, Katoma, Msalala Road, Mbugani na Uwanja imetembelewa na mratibu huyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa