Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia William Ole Nasha ameeleza kuridhishwa kwake na jinsi uongozi wa mkoa wa geita chini ya mkuu wa mkoa mhandisi Robert Gabriel juu ya usimamizi wa miradi mbalimbali ya elimu kisha kusema wizara imewezesha Shilingi Mil 152 kwa halmashauri 5 kwenye wilaya 4 za mkoa wa geita za ujenzi wa ofisi za wathibiti ubora wa elimu.
Naibu Waziri Ole Nasha ameeleza hayo agosti mosi, 2019 alipowasili mkoani geita na kufanya mazingumzo na mkuu wa mkoa wa geita akieleza dhumuni la ziara yake na kupongeza juhudi za mkoa katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa na vyoo kwa shule za msingi na sekondari, changamoto iliyojitokeza kufuatia serikali ya awamu ya tano kutoa elimu bure bila malipo iliyochochea ongezeko kubwa la wanafunzi aliposomewa taarifa ya mkoa kwenye sekta ya elimu.
“kwanza niwapongeze geita mnafanya vizuri na hakika baadhi ya mambo tutayachakua kama mfano wengine wajifunze kwani hata tathmini ya wizara inaonesha fedha zinazotolewa geita zinasimamiwa vizuri. Kama wizara tuliona madhaifu upande wa ubora wa elimu kutokana na wathibiti ubora kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha, hivyo serikali imeamua kuweka jitihada za makusudi kuboresha mifumo ya ubora wa elimu kwa kuwezesha vitendea kazi ikiwemo magari, pikipiki na sasa kujenga ofisi 100 nchi nzima ambapo geita mmepata ofisi tano katika halmashauri 5 kwenye wilaya 4 za Geita, Chato, Mbogwe na Nyang’hwale ikiwa kila ofisi imepewa shilingi Mil 152”, amesema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa amechukua ombi la mkuu wa mkoa la uanzishwaji wa chuo ya sayansi cha madaktari wilayani chato palipo na hospitali ya rufaa ya kanda kwakuwa mahitaji ya watumishi wa afya bado ni makubwa lakini vyuo vya umma na binafsi bado havitoshelezi na kwamba wizara itaendelea kusimamia ujenzi wa chuo cha VETA kutokana na kusuasua kwa ujenzi wake mkoani hapa ambapo kwa sasa ujenzi wake umesimama kutokana na madhaifu yaliyojitokeza wakati wa kumpata mkandarasi na hadi sasa suala hilo lipo takukuru.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa mhandisi Robert Gabriel amesema, kama mkoa lengo ni kutoka kwenye 48% na kufikia 62% upande wa ujenzi wa miundombinu ya elimu msingi ambapo mafanikio yanaendelea kuonekana kutokana na mashirikiano baina ya serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo bila kusahau fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii CSR kutoka mgodi wa dhahabu geita GGM ambazo zimeendelea kuleta matokeo geita kwani lengo ni kuifanya geita iwe kituo kikubwa cha elimu watu watoke pande zote kuja kusoma hapa.
Mhandisi Gabriel amemweleza Naibu waziri kuwa, wakazi wa geita wanayo kiu kubwa ya kutumia chuo cha VETA ambacho kwa sasa ujenzi umesimama hivyo kuchelewesha ndoto za wakazi hao ambapo amamemwomba kusaidia ujenzi huo kuendelea na wadeni wa mkandarasi kuhakikisha wanaliwa madeni wanayodai. Pia ameeleza mkakati wa kuwa na benki za matofali kwenye kila shule kwa lengo la kutatua changamoto ya upungufu wa vyoo.
Taarifa ya Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mwl.Yesse Kanyuma inaonesha kuwa, mkoa bado una mahitaji ya vyumba vya madarasa 9,234 ili kufikia lengo la vyumba 13,901 kwa elimu msingi, na vyumba vya sekondari 917 kati ya 2,209.
Mkoa wa Geita una jumla ya shule za msingi 634 ikiwa za serikali ni 593 na 41 za binafsi. Shule za sekondari 127 ambapo kati ya hizo, 113 ni za serikali na 14 za binafsi, vyuo vya ualimu viwili vinavyomilikiwa na watu binafsi, chuo cha ufundi kimoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambacho kina vituo geita Mjini na chato.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa