Na Boazi Mazigo-Geita
Mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela amezindua mradi wa maji utakaowahudumia wananchi 10,448 katika Vijiji vya Nzera na Bugando, kata ya Nzera, Tarafa ya Bugango, Jimbo la Geita ndani ya halmashauri ya wilaya Geita, huku akiwapongeza wananchi wa kata hiyo kuzindua mradi huo wakati nchi ikielezea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka miwili chini ya uongozi wa Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwasihi kutunza miundombinu lakini pia kuhakikisha wanaunganisha maji hadi nyumbani.
Mhe.Shigela ameyasema hayo Machi 19, 2023 katika eneo la soko la Nzera akizungumza na wananchi baada ya kutembelea na kupanda mti aina ya Mdodoma kwenye chanzo cha maji kwenye mradi huo katika kitongoji cha Lukelege unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambapo amewasihi kamati za maji wasigeuze mradi huo shamba la bibi.
“niwapongeze kuchagua kuzindua mradi siku ambayo mhe.Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan anatimiza miaka miwili madarakani, huu ni mradi kielelezo. Pia niwapongeze RUWASA kwa kazi nzuri lakini kubwa zaidi niwaombe wakazi wa Nzera tujiandae, Nzera inakuwa mji hivyo tukubali kupangwa na tuwe tayari kuchangamkia fursa baada ya ukamilishwaji wa bandari ya Nkome itakayojengwa hivi karibuni, lakini pia uwepo wa reli ya kisasa SGR pamoja na daraja la Magufuli (Kigongo-Busisi)”, alisema Mhe.Shigela
Mwisho, Mhe.Shigela alimaliza kwa kuwasisitiza wazazi kuwapeleka watoto shule wapate elimu ili kuwa na wataalam wa hapo baadaye, vilevile amewaalika kutumia huduma za afya za kibingwa zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato yenye vifaa vya kisasa kama CT-Scan, MRI, Dialysis Machine n.k pamoja na kuagiza wataalam ambao wana kero ambazo hawajazitatua kwa wananchi wafanye hivyo haraka kabla hajarudi kufanya ziara kujionea ujenzi wa barabara Km 20 kiwango cha lami katika kipande cha kwanza kutoka Nkome-Sungusila.
Naye mbunge wa jimbo la Geita Mhe.Joseph Kasheku Msukuma alisema, anaipongeza sana RUWASA na kwamba katika jimbo hilo miradi mingi ya RUWASA inaendelea kutekelezwa hivyo kutumia fursa hiyo kuyasema mafanikio ya serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwasihi wananchi kuchangia huduma ya maji kwa kujisajili ili waunganishiwe maji huku akiwataka wananchi anaowaongoza kuyapa mkono maendeleo na si kuyapinga.
Akisoma taarifa ya mradi Meneja wa RUWASA Wilaya Geita Mhandisi Sande Batakanwa alisema, mradi huo wa kisima kirefu una kina cha Mita 50 chenye uwezo wa kuzalisha lita 3,600 za maji kwa saa pamoja na mtandao wa bomba wenye urefu wa Km. 6.679 na ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji. Mradi ulianza kutekelezwa Desemba 2021 na ulikamilika Desemba 2022 na utahudumia wananchi zaidi ya 10,448 kwa gharama ya shilingi milioni mia mbili tisini na tatu na elfu hamsini na mia tano na nane na senti hamsini na nane (293,050,508.58) kutoka katika chanzo cha Mapambano dhidi ya UVIKO-19
Mhandisi Batakanwa aliongeza kuwa, ukamilikaji wa mradi huo unapunguza muda uliokuwa unatumiwa na wananchi kufuata maji umbali mrefu ambapo kwa sasa muda huo utatumika kwenye kujenga uchumi. Vilevile, utapunguza magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama kama vile kuhara, homa ya matumbo na kipindupindu, lakini kubwa zaidi kufungua fursa za kiuchumi kama uendeshaji viwanda vidogo na bustani za mbogamboga.
Sherehe hizo za uzinduzi zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwemo kamati ya usalama mkoa, viongozi wa CCM Wilaya na Kata pamoja na watumishi wa RUWASA Mkoa na Wilaya.
Geita, Hakuna Kilichosimama
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa