Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko amezindua rasmi mradi wa kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi katika maeneo yaliyopitiwa na Bomba la mafuta Ghafi la Afrika Mashariki unaotarajiwa kuwanufaisha Zaidi ya vijana elfu 12.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika katika Uwanja wa kijiji cha Bukombe Wilayani Bukombe Geita tarehe 18 Septemba 2025 Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zitokanazo na Bomba la mafuta ghafi katika mikoa ya Geita, Kagera, Tabora na Tanga kwa awamu ya kwanza.
Dkt Biteko amesema mradi huo ni sehemu ya kuongeza mnyororo wa thamani katika mradi wa EACOP ambapo juhudi zote hizi ni kuhakikisha mradi unaleta manufaa kwa jamii na kusaidia kupunguza umasikini wa watu na kuwaasa vijana waliopata fursa kwenye mradi wa EACOP kulinda raslimali za kampuni na kuwajibika kwa matakwa ya mkataba ili wawe mabalozi wa watanzania.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa hadi Julai 2025, serikali imewekeza takribani sh Trillioni 1.125 na kusaidia mradi kutoa ajira 9,194 za moja kwa moja ikiwemo vijana 170 waliofadhiliwa masomo ya ujuzi na ufundi stadi na kisha kuajiriwa. Kadhalika kampuni imetoa ufadhili wa vijana 238 kwa ajili ya kwenda kusoma kwenye vituo mbalimbali nchini, haya yote ni manufaa ya mradi huu tunaouzungumza hapa.
Meneja Uwajibikaji na Uwekezaji kwa Jamii wa EACOP Bi. Clare Haule amesema programu ya uwezeshaji vijana kiuchumi inazingatia fursa kwa vijana, huduma za maji, afya na usalama wa jamii, nishati endelevu na mazingira na kueleza kuwa katika awamu ya kwanza ya program ya uwezeshaji vijana itanufaisha mikoa minne ambayo ni Geita, Kagera, Tabora na Tanga kati ya mikoa nane inayopitiwa na mradi wa EACOP.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EACOP, Geofrey Mponda amesema hadi kufikia mwishoni mwa robo ya mwaka 2025 zaidi ya asilimia 80 ya ajira katika mradi zimejazwa na wazawa kutoka Tanzania na Uganda.
Ndg. Mponda amefafanua kuwa serikali imetoa muongozo kuhakikisha mpango wa ajira za kigeni inaendana na makubaliano ya wanahisa na watanzania wanapewa kipaumbele katika nafasi za kazi zinazohitajika na kampuni ya EACOP na kueleza kuwa mwaka 2024 EACOP ilianzisha mafunzo maalum na kuweza kudahili watanzania vijana 112 na waganda 29 walipata fursa ya kufanya mafunzo ya nadharia na vitendo na baada ya kuhitimu wataajiriwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa wa Geita itaendelea kushirikiana na wataalam wanaofanya kazi katika mradi wa Bomba la mafuta na kueleza baadhi ya faida zinazopatikana kupitia mradi huo ni pamoja na wananchi kunufaika na mnyororo wa thamani kwa kufanya biashara mbalimbali pamoja na ajira za muda mfupi na mrefu kwa jamii .
Tangu kuanza ujenzi wa mradi wa Bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki jumla ya kampuni 200 za kitanzania zimepata zabuni katika mradi huo ambao umefikia asilimia 65 ya utekelezaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa