ZOEZI LA UOGESHAJI MIFUGO LAZINDULIWA RASMI GEITA
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu. Mohamed Gombati amezindua rasmi zoezi la uogeshaji mifugo ambalo linafanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Geita.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kimkoa katika josho la Kasamwa Halmashauri ya Mji Geita tarehe 03/7/2024, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia mkoa wa Geita ruzuku ya lita 839 za dawa aina ya Roll dip kwa ajili ya kuoshea mifugo.
Ndg. Mohamed Gombati ameeleza kuwa ruzuku hiyo iliyotolewa na Serikali inadhihirisha namna Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyo na nia ya dhati ya kuwainua wafugaji walioko katika mkoa wa Geita kiuchumi na kuendeleza sekta ya mifugo kwa ujumla.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita amesema kuwa zoezi la uogeshaji mifugo litakinga mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo dhidi ya magonjwa yaenezwayo za kupe pamoja na mbung’o , ukurutu wa ngozi na kuwa na mifugo yenye afya bora itakayowapatia fursa tele za kibiashara zitokanazo na mifugo.
Ndg. Gombati ametoa pongezi kwa wafugaji wote walioshiriki katika ukarabati na ujenzi wa majosho katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wa Geita, ambapo wanakamati wa majosho walifanya shughuli kama ubebaji mchanga, kokoto na kuchimba mashimo ya kujengea matenki ya majosho.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ametoa agizo kwa Halmashauri zote ndani ya Mkoa kuhakikisha malambo ya maji yanajengwa, majosho yanayohitaji marekebisho yarekebishwe ndani ya mwaka mpya wa fedha 2024/2025 na njia za kupitishia mifugo (mapanda) zizibuliwe ili kuruhusu mifugo kufika kwa urahisi kwenye majosho
Ndg. Mohamed Gombati ametumia fursa hiyo kuwaasa wataalam wa idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuwatembelea wafugaji mara kwa mara kwa lengo la kuwasaidia kufuga kibiashara na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Daktari wa mifugo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, David Misonge ameeleza kuwa zoezi hilo ni endelevu ambapo uogeshaji katika Mkoa wa Geita ulianza mwaka 2019 baada ya kampeni ya uogeshaji kuzinduliwa rasmi mwezi Oktoba mwaka huo. Mwongozo kuhusu uogeshaji mifugo ulitolewa na unafuatwa ambapo kamati za wafugaji zimeshaundwa na zinaendesha majosho hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji na wanakamati wa josho la Kasamwa, Sylvester Ng’honoli ametoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia dawa ya ruzuku kwa ajili ya kuendeleza zoezi la kuogesha mifugo na kutoa ombi kwa Serikali kutatua changamoto ya kukosekana kwa njia za kupitisha mifugo kunakopelekea baadhi ya wafugaji kushindwa kuogesha mifugo yao kwa malalamiko ya kukosa njia (mapanda).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa